Wednesday, April 18, 2012

JICHUNGE NA UCHOVU WA DUNIA

Shalom.Tumepewa zawadi ya kuishi hapa duniani kila mtu kwa namna yake.Hatufanani.Lakini ingawa hatufanani bado neema ya Mungu iko kwa kila mmoja wetu ili atimize mapenzi ya Mungu katika maisha yake.Dunia imejaa uchovu.Kelele juu ya njaa,kutaka sifa,mali,uovu na kila hitaji kwa watu liwe baya au zuri.Maisha yamezungukwa na kelele.Zilikuwepo kwa wakale waliotutangulia na zinaendelea hata sasa.Hatimaye hata kesho zitaendelea kuwepo.Kitabu cha Mhubiri kinaelezea kelele hizi kama ifuatavyo-"Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka,jicho halishibi kuona,wala sikio halikinai kusikia.Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako;na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka;wala jambo jipya hakuna chini ya jua.Je kuna jambo lolote ambalo watu husema juu yake,Tazama ni jambo jipya?Limekwisha kuwako,tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi."(Mhubiri 1:8-10)
Uwe makini kwa yale unayoona na kusikia.Toa nafasi kwa yale tu yenye faida kwako.Mambo ambayo hayatakuletea uchovu wa kuwa mbali na Mungu wako.Usifungue masikio yako kwa sauti zitakazokutia katika giza la majuto.Dunia imejaa uchovu mwingi.Wakati wote inatafuta watu wa kuzama katika uchovu huo ili wawe katika mahangaiko.Jichunge.Mungu akupe nguvu na mwanga wa kuona giza lililoko duniani.Ruhusu maagizo ya Mungu yawe dira yako.Yafanyie kazi.Ishi kwayo kama ramani yako katika safari ya maisha.Mtunga zaburi aliandika,"Neno lako ni taa ya miguu yangu,Na mwanga wa njia yangu"(Zaburi 119:105).Ubarikiwe.Roho Mtakatifu akuongoze katika kila hatua ndani ya dunia hii iliyojaa uchovu.Tuombe Mungu taa ya neno lake ituongoze.Amina.

Friday, April 13, 2012

KWENU NI KWENU

Hakuna aliyekuja duniani kwa bahati mbaya."Mimi nimezaliwa hapa kwa bahati mbaya" Utasikia mtu akitamba na kujisifia.Mungu hakukosea wewe kuzaliwa mahali ulipo.Alijua unahitajika kuwepo mahali ulipo.Wa namna yako hayupo dunia nzima.Angelikuwepo usingezaliwa.Kuna vitu vizuri ameweka ndani yako kwa ajili ya utukufu wake na kwa faida ya wengine.Usijidharau.Ona fahari ya Taifa lako.Tulia na kutafakari juu ya vitu vizuri ambavyo Mungu ameweka ndani yako.Mwombe Mungu akupe fursa ya kuchipuka na kutumika hata kwa kile ambacho wewe unaona ni kidogo.Tumia elimu,kipaji,utajiri na chochote ulicho nacho kama mchango na wajibu kwa dunia inayokuzunguuka.Furahi.Jinsi ulivyo ni pambo mbele za Mungu.Usijidharau.(Zaburi 139:14-18)